DAR ES SALAAM-TANZANIA.
WAZIRI Mkuu mstaafu Kassim Majaliwa amezindua rasmi msimu wa 25 wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, akizipongeza kwa mchango wake katika kukuza michezo, utalii wa michezo na uchumi wa Tanzania.
Uzinduzi huo umefanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam, ukiashiria maandalizi ya maadhimisho ya miaka 25 ya mbio hizo, yanayotarajiwa kufanyika Februari 7, 2027, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema Kilimanjaro Marathon imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya wanariadha wa ndani, kuhamasisha utamaduni wa michezo na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
"Mbio hizi zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi kupitia shughuli mbalimbali zinazochochewa na wageni, washiriki na wadau wanaohudhuria tukio hilo."alisema.
Aliwahimiza washiriki na wageni kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii nchini, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro na Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Kilimanjaro Premium Lager, Khensani Mkhombo, alisema kampuni hiyo inajivunia kushirikiana na mbio hizo kwa miaka 25, akieleza kuwa ushirikiano huo ni miongoni mwa udhamini wa muda mrefu katika sekta ya michezo nchini.
“Kwa miaka 25, Kilimanjaro Premium Lager imesimama bega kwa bega na tukio hili la kiwango cha kimataifa kusherehekea utamaduni wa Kitanzania, michezo na roho ya jamii iliyo hai,” alisema Mkhombo.
Naye mwakilishi wa Kampuni ya YAS, Woinde Shisael, alisema kampuni hiyo itaendelea kuwezesha mbio hizo kupitia udhamini wa Mbio za Nusu Marathon, huku akibainisha kuwa huduma za mtandao wa 4G na 5G zinasaidia kuunganisha washiriki na wadau mbalimbali.
Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa CRDB Bank, Muhumuliza Buberwa, alisema benki hiyo inajivunia kuendelea kudhamini Mbio za Kujifurahisha za Kilomita Tano (Fun Run), zinazotoa fursa kwa familia, vijana na wakimbiaji wanaoshiriki kwa mara ya kwanza kuwa sehemu ya tukio hilo.
Waandaaji wa mbio hizo, Kilimanjaro Marathon Company Limited, wamethibitisha kuwa usajili katika makundi yote utafuata utaratibu wa anayewahi ndiye anayehudumiwa kwanza.
Mbio hizo za msimu wa 25 zinatarajiwa kuwakutanisha wanariadha, familia na washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kuadhimisha safari ya miaka 25 ya mashindano hayo.









