DIWANI AJENGA KIVUKO KUONDOA ADHA YA WANANCHI MIEMBENI


MIEMBENI-MOSHI.

WANANCHI wa Mtaa wa Mjimwema, Kata ya Miembeni, Manispaa ya Moshi, wameondokana na adha ya kuvuka mto wakati wa mvua baada ya kujengewa kivuko kilichokuwa kimekuwa changamoto kwao, hasa katika kipindi cha masika ambapo maji hujaa na kuwa na mkondo mkubwa uliotishia usalama wa maisha yao.

Wakizungumza na *Kisenaupdated.blogspot.com* wananchi hao wamesema awali walikuwa wakikabiliwa na hofu kila walipolazimika kuvuka mto huo, wakiwemo watoto waliokuwa wakishindwa kwenda shule, wazee na akina mama wajawazito kutokana na hatari ya kusombwa na maji.

Mwanaisha Hamishi, Deo Msacky na Husna Rashi, walisema kukamilika kwa kivuko hicho kumekuwa mwarobaini wa changamoto hiyo, kwani sasa wanaweza kuvuka kwa urahisi na kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu kubwa iliyokuwa ikiwakabili wakati wa mvua.

Diwani Kata ya Miembeni  Haruna Ally Mushi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Miembeni, Haruna Ally Mushi, alisema kivuko hicho kilikuwa na mbao zilizokuwa zimeoza, hali iliyofanya matumizi yake kuwa hatarishi na kuwasababishia wananchi changamoto kubwa, hasa wakati wa mvua.

Haruna ambaye pia ni Katibu wa Madiwani wa (CCM) Moshi Mjini, amesema alifanya jitihada za kuomba fedha kupitia Mfuko wa Jimbo na kufanikiwa kupata Sh milioni tano kwa ajili ya kukarabati kivuko hicho, hata hivyo, kutokana na hali ya mbao zilizokuwapo awali kuoza, aliamua pia kufanya jitihada zake binafsi ili kuhakikisha kivuko hicho kinajengwa kwa vyuma, ili kivuko hicho kiweze kudumu na kuwasaidia wananchi kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mjimwema, Paulo Minja, alimshukuru diwqni huyo kwa hatua hiyo, akisema kukamilika kwa kivuko hicho kumesaidia kuondoa kikwazo kilichokuwa kikiwakabili wananchi, hususan wanafunzi waliokuwa wakishindwa kuvuka kwenda shule wakati wa masika.

Alisema kivuko hicho kina umuhimu mkubwa kwa kuwa kinaunganisha Kata za Njoro na Miembeni ndani ya Manispaa ya Moshi, hivyo kukamilika kwake kunatarajiwa kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wa maeneo hayo.

8






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.