MOSHI-KILIMANJARO
MAAFISA ugani wqmeqgizwa kuacha kukaa maofisini na badala yake kwenda mashambani kuwaongoza wakulima kutumia kanuni bora za kilimo cha kahawa na miche bora iliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), ili kuongeza uzalishaji na tija ya zao hilo.
Kauli hiyo ilitolewa Oktoba 10,2026 na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava, wakati akifunga Tamasha la Saba la Kahawa lililofanyika katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa (TCCCO), kilichopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo alisisitiza umuhimu wa maafisa ugani kusimamia na kuwaelekeza wakulima matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa za kilimo cha kahawa.
Alisema maafisa ugani wanapaswa kuwafikia wakulima katika mashamba yao na kuwasaidia kutumia miche bora inayovumilia ukame na kustahimili magonjwa, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji na kukuza mnyororo wa thamani wa zao hilo.
“Maafisa ugani wetu, tokeni maofisini, nendeni mashambani mkawasaidie wakulima ambao ndio wazalishaji, ili waweze kutumia kanuni bora za kilimo cha kahawa na miche bora iliyofanyiwa utafiti,” alisema Mnzava.
Aliongeza kuwa, ili kahawa ya Tanzania iweze kunufaisha zaidi wakulima na wadau wengine, ni muhimu kuongeza thamani ya zao hilo kupitia usindikaji, ufungashaji na utengenezaji wa bidhaa zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa wadau wa kahawa wanapaswa kuelewa mahitaji ya soko ili bidhaa zinazozalishwa ziendane na viwango na matakwa ya wanunuzi.
Pia aliwataka wadau wote katika mnyororo wa thamani wa kahawa kuwekeza katika kukuza soko la ndani kwa kuhamasisha Watanzania kutumia kahawa inayozalishwa nchini, akisema hatua hiyo itasaidia kujenga soko la uhakika kwa wakulima.
Aidha, aliitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuendelea kuwashirikisha vijana na wanawake katika uzalishaji na shughuli za kuongeza thamani ya zao hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCB, Profesa Aurelia Kamuzora, alisema mkakati wa kukuza biashara ya kahawa nchini umeendelea kuchochewa na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ikiwemo miamala kupitia simu za mkononi na mifumo ya ufuatiliaji wa shughuli za uzalishaji na biashara ya kahawa.
Alisema matumizi ya mifumo hiyo yamechangia kuongeza imani ya wakulima, wakiwemo vijana, katika shughuli za uzalishaji wa kahawa.
Aliongeza kuwa TCB inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa zao hilo kutangaza chapa ya kahawa ya Tanzania ili kuongeza ushindani na kuvutia masoko zaidi ya kimataifa.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Denis Mahulu, alisema maonyesho hayo yanaendelea kukua kila mwaka, akibainisha kuwa mwaka huu yalishirikisha washiriki zaidi ya 40, hali inayoonesha kuongezeka kwa ushiriki wa wadau tangu tamasha hilo lilipoanzishwa.







