Diwani Wa Kata ya Bondeni Alhaj Fundi, akishiriki kufanya usafi katika maeneo ya Soko Kuu la Mbuyuni.
MOSHI-KILIMANJARO.
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wameshiriki zoezi la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya kata zao, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na mvua zinazotarajiwa kunyesha.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumu, amesema ameshirikiana na wananchi wa Mtaa wa Viwanda kufanya msaragambo wa kuondoa tope katika Mto Njoro, ambao umekuwa ukisababisha mafuriko na kuathiri familia zinazoishi maeneo ya jirani wakati wa mvua.
Kidumo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Njoro, amesema ushiriki wa wananchi katika kusafisha maeneo yanayozunguka makazi yao ni muhimu kwa kuwa utasaidia kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na maji ya mvua , ikiwemo kuziba kwa njia za maji na mafuriko.
Diwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, amesema tayari wameanza kusafisha mitaro na kuondoa tope katika mifereji ya maji ya mvua kwa kushirikiana na wananchi, huku akiwataka wananchi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka.
Naye Diwani wa Kata ya Bondeni, Haji Fundi Haji, amewataka wafanyabiashara wa Soko la Mbuyuni kuhakikisha maeneo yao ya biashara yanakuwa safi na kutupa taka katika maeneo yaliyotengwa, ili kuepuka kuziba njia za maji.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Korongoni, Ussah Bulilo, amesema ameshiriki zoezi hilo kwa lengo la kuhakikisha kata yake inakuwa safi na salama, huku akiwataka wananchi kuendelea kufanya usafi mara kwa mara.
Madiwani hao wamesema usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja, hivyo wamewataka wananchi na wafanyabiashara kushirikiana na viongozi katika kusafisha mitaro na maeneo yanayozunguka makazi na biashara.
Wamesema hatua hiyo itasaidia kuzuia taka na tope kuziba mitaro na mifereji ya maji, jambo ambalo linaweza kusababisha maji kutuama na kuongeza athari za mafuriko wakati wa mvua.
![]() |













