Diwani wa Kata ya Njoro Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, akishiriki na wqnanchi katika kuchimba udongo ikiwa ni jitihada za kuurejesha Mto Njoro katika njia yake ya asili.
NJORO-MOSHI.
BODI ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), imeanza jitihada za kuurejesha Mto Njoro katika njia yake ya asili, baada ya mto huo kujaa tope na kubadili mkondo wake, hali inayosababisha maji kuelekea katika makazi ya wananchi na kuongeza hatari ya mafuriko.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakazi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa Mto Njoro kukumbwa na mafuriko mara kwa mara, kutokana na maji yanayotoka maeneo ya juu na katikati ya Mji wa Moshi kushindwa kupita katika mkondo wa asili wa mto huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la uchimbaji na uondoaji wa tope katika Mto Njoro, Mtaalamu wa Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), Brown Mwangoka, amesema kujaa kwa tope kumesababisha mto huo kupoteza sehemu ya njia yake ya asili na maji kuelekea katika maeneo ambayo yana makazi ya wananchi.
Mwangoka amesema awali Bodi hiyo ilishirikiana na Diwani wa Kata ya Njoro ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Kidumo, kuleta mitambo ya kuondoa tope hilo, ikiwemo excavator, lakini kazi hiyo ilikwama kutokana na eneo hilo kuwa na udongo laini na chepechepe.
Amesema kutokana na hali hiyo, Bodi ya Maji Bonde la Pangani na uongozi wa Kata ya Njoro wameamua kushirikisha wananchi katika kazi hiyo kwa kutumia majembe na mabeleshi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na mvua zinazotarajiwa.
Mwangoka amesema shughuli za binadamu, ikiwemo kilimo karibu na mto pamoja na ujenzi wa makazi, zimechangia mto huo kujaa tope na kupoteza njia yake ya asili, hivyo kuna umuhimu wa kuchukua hatua ili kurejesha mkondo wa maji na kupunguza hatari ya mafuriko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa Mtaa wa Viwanda, Isaack Kabengwe, amesema eneo hilo limekuwa likikumbwa na mafuriko mara kwa mara, hivyo wananchi wameunga mkono zoezi hilo kama sehemu ya maandalizi ya mvua.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwanda, Osward Nkindi, amesema shughuli za kilimo ndani ya mita 60 kutoka kwenye mto pamoja na ujenzi wa makazi vimechangia mto huo kujaa tope na kuacha njia yake ya asili.
Baadhi ya wakazi wa Viwandani, Steven Maimu, Abubakar Fungameza na Mawaisha Shabani, wamesema maji yanayotoka Mto Rau pamoja na kwenye makorongo yamekuwa yakielekea katika maeneo wanayoishi na kusababisha mafuriko, hivyo ameupongeza mpango wa kusafisha Mto Njoro ili maji yarudi katika njia yake ya asili.
Akizungumza katika zoezi hilo, Meya wa Manispaa ya Moshi na Diwani wa Kata ya Njoro, Mhandisi Zuberi Kidumo, amesema wananchi wameamua kufanya msaragambo wa kuondoa tope katika mto huo, akisema mafuriko yamekuwa yakisababisha athari kwa familia nyingi kila kipindi cha mvua.
Kidumo ameishukuru Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), kwa kushirikiana na wananchi katika zoezi hilo, akisema kurejeshwa kwa njia ya asili ya Mto Njoro kutasaidia maji kutoka maeneo ya juu kupita katika mkondo wake na kupunguza uwezekano wa kuelekea katika makazi ya wananchi.












