KIJANA KWANZA FC YATWAA UBINGWA MAULID CUP KILIMANJARO


MOSHI-KILIMANJARO.


TIMU ya Kijana Kwanza FC ya Moshi Mjini imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Maulid Cup baada ya kuichapa Kikavu FC ya Hai mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Railway, Moshi.

Ushindi huo umeifanya Kijana Kwanza FC kutwaa taji hilo katika mashindano yaliyoandaliwa na The Bilal Muslim Mission of Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro, yaliyolenga kuadhimisha Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), huku kundi kubwa la walengwa likiwa ni vijana.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya timu 12 kutoka wilaya za Moshi Mjini, Moshi Vijijini, Siha, Hai na Mwanga, ambazo zilianza safari ya kusaka ubingwa kupitia hatua ya makundi kabla ya kufika hatua za mtoano na hatimaye fainali.

Kijana Kwanza FC ilitawala mchezo wa fainali na kutumia vyema nafasi ilizopata, na kufanikiwa kupata mabao mawili yaliyoiwezesha kuondoka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Kikavu FC.

Mwenyekiti wa Kijana Kwanza FC, Mujibu Abeid, ameipongeza timu yake kwa ushindi huo, akisema mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano, juhudi na nidhamu iliyojengwa miongoni mwa wachezaji.

Abeid ameishukuru The Bilal Muslim Mission of Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuandaa mashindano hayo, akisema yamewapa vijana fursa ya kuonyesha vipaji vyao, kukutana na kujenga urafiki na mshikamano kupitia michezo.

Amesema Kijana Kwanza FC itaendelea kuunga mkono juhudi za kuwaendeleza vijana kupitia michezo, huku akiwataka wachezaji kutumia vipaji vyao kwa bidii, nidhamu na kuheshimu viongozi, waamuzi pamoja na timu pinzani.

Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mashindano hayo alikuwa Chief Mlindoko, mlezi wa The Bilal Muslim Mission of Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza katika hafla hiyo, Chief Mlindoko aliipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa mashindano hayo, akisema michezo ni nyenzo muhimu katika kuwaunganisha vijana, kukuza vipaji na kuwajengea nidhamu.

Katika utoaji wa zawadi, Kijana Kwanza FC ilikabidhiwa seti ya jezi, kikombe, mpira na Shilingi 150,000, huku Kikavu FC iliyomaliza nafasi ya pili ikipata mpira na Shilingi 100,000.

Aidha, timu ya Under 17 iliyoshiriki mashindano hayo ilikabidhiwa seti ya jezi, huku timu iliyofanya vizuri kwa upande wa nidhamu nayo ikizawadiwa seti ya jezi.

Mchezaji aliyeibuka Fair Player pia alikabidhiwa seti ya jezi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha vijana kuzingatia nidhamu na uchezaji wa kiungwana.

Mashindano ya Maulid Cup yamekuwa jukwaa la kuwakutanisha vijana kutoka wilaya mbalimbali za Kilimanjaro, huku kauli mbiu ya ujumbe wa Maulid ni "Matumizi ya Michezo katika Kujenga Mshikamano, Kukuza vipaji na Kuhamasisha Vijana Kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa Jamii."












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.