CCM KUWANYANG'ANYA KADI VIONGOZI WANAOZALISHA MIGOGORO



MOSHI-KILIMANJARO.

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopewa dhamana ya kuwaongoza wananchi wametakiwa kushuka katika maeneo yao, kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili, badala ya kujihusisha na migogoro na malumbano yanayoweza kukidhoofisha chama.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Agrey Mwanri, alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na wananchi, viongozi wa chama na serikali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Manyema, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kichama mkoani humo.

Mwanri alisema CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wanaoendelea kugombana na kushindwa kutatua changamoto za wananchi waliowachagua, akisisitiza kuwa viongozi hao wamepewa dhamana ya kuwahudumia wananchi na si kuwasababishia migogoro.

Alisema wananchi wamekuwa wakifika kwa viongozi mbalimbali wakiwa na nyaraka zinazoeleza kero zao, lakini baadhi ya viongozi wakiwemo wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani na wabunge, wamekuwa wakishindwa kuzifanyia kazi changamoto hizo, hali inayowafanya wananchi kuendelea kuteseka.

Mwanri alisema CCM imekuwa ikiwapatia viongozi hao nafasi na dhamana kupitia chama, hivyo haiwezi kuvumilia hali ya viongozi kutumia nafasi walizopewa huku wakishindwa kuwahudumia wananchi.

“Kama kuna viongozi wanaendelea na mchezo huu, sisi kama chama tutakuwa wakali kweli kweli, tiketi uliipata kwetu, na kama sisi ndio tuliokupa tiketi hiyo, hatutakawia kukunyang’anya,” alisema Mwanri.

Aidha, Mwanri alisisitiza umuhimu wa viongozi kushuka chini na kukutana na wananchi katika maeneo wanayoishi, badala ya kukaa maofisini na kusubiri wananchi wafike kuwafuata.

“Tunataka vikao kama mwenyekiti wa mtaa, kule kwako hatutaki kusikia unakaa ofisini. Shuka kwa wananchi, wasikilize na uwatatulie changamoto zao,” alisema.

Alisema CCM imepokea maelekezo na maagizo yaliyotolewa na viongozi mbalimbali waliowahi kufanya ziara mkoani Kilimanjaro, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Steven Wasira, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba pamoja na aliyekuwa Mlezi wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Rabia, na kwamba chama kinaendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo.

Mwanri alisema CCM itaendelea kufuatilia utendaji wa viongozi waliokabidhiwa dhamana ya kuwaongoza wananchi ili kuhakikisha kero na changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Akozungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi alisema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi umeendelea kutekelezwa kikamilifu katika Mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu alisema katika kipindi cha miaka mitano serikali imetoa Sh 1.5 Trilioni katika Mkoa huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema mbali na fedha hizo katika mwaka wa fedha 2026/2027 serikali imetoa Sh 33bilioni kwa ajili ya kumalizia mradi wa umeme katika vitongoji 189 vilivyobakia.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.