KILI PLANTATION FC, HAI UNITED KUKIPIGA KESHO NUSU FAINALI ZUBERI CUP

MOSHI-KILIMANJARO. 

NUSU FAINALI ya Mashindano ya Zuberi Cup inatarajiwa kuchezwa kesho Jumapili, Agosti 16, mwaka huu, kati ya Kili Plantation FC na Hai United katika Uwanja wa Railway Njoro, Moshi, kuanzia majira ya saa 10:00 jioni.

Mpambano huo unatarajiwa kuwa mkali kutokana na ubora wa timu hizo mbili, huku Hai United ikiingia uwanjani ikiwa na morali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fire FC katika mchezo wa robo fainali na hivyo kufuzu hatua ya nusu fainali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Japhet Mpande, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mchezo huo, akieleza kuwa mashabiki wanatarajiwa kushuhudia mchezo wenye ushindani mkubwa kutokana na timu zote kuwa na malengo ya kutinga fainali.


Kwa upande wake, Kili Plantation FC imefuzu hatua hiyo baada ya kuiondoa Kibo Warriors FC kwa mikwaju ya penalti 5-3, katika mchezo wa robo fainali uliokuwa na ushindani mkubwa.

Mpande amesema mshindi wa mchezo huo ataendelea na safari ya kuwania ubingwa wa Zuberi Cup, huku mchezo wa kuwania nafasi ya tatu ukitarajiwa kuchezwa Agosti 22, mwaka huu, kabla ya fainali ya mashindano hayo kuchezwa Agosti 23.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.