SSAMIA ATAKA UTAFITI WA KINA KUBAINI CHANZO CHA WATOTO KUZALIWA NA MATUNDU YA MOYO

MOSHI-KILIMANJARO.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka watafiti wa afya nchini kushirikiana na wataalamu wa kimataifa kufanya tafiti za kina ili kubaini sababu za ongezeko la watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo, hususan matundu ya moyo, na kutoa elimu sahihi kwa jamii ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa Jengo la Huduma za Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, lililogharimu zaidi ya shilingi bilioni 17, ikiwemo gharama za vifaa tiba.

Alisema taarifa alizopewa zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wa moyo wanaopatiwa huduma katika KCMC wanatoka Kanda ya Kaskazini, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi ili kubaini chanzo chake.

“Watafiti wetu wa afya kwa kushirikiana na wataalamu wa kimataifa waangalie kwa kina sababu zinazochangia watoto kuzaliwa na matatizo ya moyo, tufahamu ni nini kinachosababisha ongezeko hili na tutoe elimu ya kutosha kwa Watanzania ili kuzuia sababu zinazoweza kuwaletea watoto maradhi haya,” alisema Rais Samia.

Alieleza kuwa kukamilika kwa jengo la kisasa la magonjwa ya moyo linalojengwa KCMC kutasaidia wagonjwa wengi kupata huduma karibu na makazi yao badala ya kusafiri kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia huduma za saratani, Rais Samia alisema ugonjwa huo si changamoto ya mtu mmoja, familia au kundi fulani la watu, bali ni tatizo linaloigusa jamii nzima na kuathiri uchumi pamoja na ustawi wa taifa.

“Changamoto hii haishii kwenye matibabu pekee. Huleta hofu kwa familia, gharama kubwa za matibabu, safari ndefu na wakati mwingine kuvunja ndoto za familia. Nyuma ya kila mgonjwa kuna familia inayohangaika na Mtanzania anayehitaji kurejeshewa matumaini,” alisema.

Alisema Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kwa kuanzisha vituo vya matibabu ya saratani na huduma za upasuaji wa moyo katika kanda mbalimbali za nchi ili kupunguza msongamano katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuanzishwa kwa huduma za saratani KCMC ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa rufaa nchini na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo jirani.

Alisema Serikali imechangia shilingi bilioni 5.5 katika ujenzi wa jengo hilo la saratani na imeahidi kulifanyia kazi ombi la awamu ya pili la vifaa tiba ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa zaidi.

Aidha, aliupongeza uongozi wa KCMC kwa juhudi za kuboresha huduma za afya na kusisitiza umuhimu wa wagonjwa kupokelewa kwa wakati, kufanyiwa vipimo bila kucheleweshwa, kupewa maelezo sahihi kuhusu matibabu yao na kufuatiliwa ipasavyo baada ya kupata huduma.


Rais Samia alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga takribani shilingi trilioni 1.8 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vya sekta ya afya, ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma, dawa na vifaa tiba.

“Tunawekeza katika afya kwa sababu uwekezaji katika afya ni uwekezaji katika nguvu kazi ya taifa na ustawi wa familia, Malengo ya maendeleo ya miaka 25 ijayo hayawezi kufikiwa kama hatutakuwa na wananchi wenye afya njema na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi,” alisema.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.