NACTVET YAHUISHA MITAALA YA FITI KUKIDHI MAHITAJI YA SOKO

                                               MOSHI-KILIMANJARO

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeanza mchakato wa uhuishaji wa mitaala ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI), kwa lengo la kuhakikisha mitaala hiyo inalingana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira, maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya sekta ya misitu nchini.

Akizungumza wakati wa warsha ya kupitia mitaala ya chuo hicho kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Afisa Mdhibiti Ubora Mkuu wa Mitaala kutoka NACTVET, Dkt. Edward Joseph Mneda, alisema mitaala hiyo ilikuwa ikitumika kwa zaidi ya miaka mitano na sasa inafanyiwa mapitio ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kitaaluma.

“Mitaala tunayohuisha sasa inalenga kutoa mafunzo ya vitendo zaidi ili kuhakikisha kijana anayehitimu kutoka FITI ana uwezo wa kujiajiri, si kusubiri ajira,” alisema Dkt. Mneda, akibainisha kuwa mapitio hayo yanahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya misitu, mazingira na viwanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha FITI, Dkt. Lupala Zacharia, alisema chuo hicho sasa kimepata kibali maalum cha kudahili wanafunzi watakaonufaika na mikopo ya asilimia 100 kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kwa wale wanaojiunga na Astashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu.

“Hatua hii ni muhimu sana kwa vijana, kwa kuwa awali wanafunzi wa FITI hawakuwa wakipata mikopo. Serikali sasa inatambua mchango wa elimu ya misitu katika maendeleo ya uchumi wa kijani,” alisema Dkt. Lupala.

Aliongeza kuwa tayari chuo kina afisa mikopo maalum aliyewekwa kusaidia wanafunzi kukamilisha taratibu zote ili kunufaika na mikopo, na kwa wanafunzi walioko chuoni, asilimia 50 yao tayari wameanza kupokea mikopo kupitia HESLB.

Katika hatua nyingine, FITI pia kimepewa kibali cha kuendesha mafunzo ya ufundi kupitia VETA, yakiwemo masomo ya useremala, ufundi wa isitu na uchakataji wa mazao ya misitu. mafunzo haya yanawalenga vijana waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari na kuwapa fursa ya kupata ujuzi wa kujiajiri.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Edward Kohi, alisisitiza kuwa mchakato wa kuhuisha mitaala na uwekezaji katika FITI ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuandaa vijana wenye taaluma ya kisasa katika bidhaa za misitu zilizohandisiwa.

“Tunataka kuona vijana wanakuwa wabobezi katika kutengeneza bidhaa za mbao zenye viwango vya kimataifa, hili litaongeza ajira na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi,” alisema Kohi.

Serikali kupitia ushirikiano na nchi ya Ufini (Finland) na vyuo kutoka Ulaya, inaendelea kuwekeza kwenye FITI kupitia mafunzo ya walimu, miundombinu ya kisasa, na maabara za kutathmini ubora wa mbao na vifaa vingine vya misitu.

Dkt. Lupala alihitimisha kwa kutoa wito kwa vijana wa Kitanzania kuchangamkia fursa zilizopo chuoni hapo, akisema kuwa FITI ni kitovu cha elimu ya amali inayojikita katika ujuzi, ubunifu na ajira kwa vijana wa sasa na baadaye.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.