CCM AJIVUNIA USHINDI WA VIJIJI 510, YAELEZA FEDHA TRILIONI 1.4 ZILIZOTEKELEZA MAENDELEO KILIMANJARO MOSHI-KILIMANJARO

                                        MOSHI-KILIMANJARO.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza mafanikio makubwa ya ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana mkoani Kilimanjaro chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kikitaja zaidi ya vijiji 510 na vitongoji 2,227 kuwa chini ya CCM                          

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Soko la Manyema mjini Moshi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, Selemani Mfinanga, alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Manispaa ya Moshi, CCM ilifanikiwa kuchukua mitaa yote 60.

“Mkoa wa Kilimanjaro una vijiji 519, kati ya hivyo tulishinda vijiji 510, tunavyo vitongoji 2,257 na kati ya hivyo tulishinda vitongoji 2,227,” alisema Mfinanga huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara uliohutubiwa pia na Katibu wa NEC wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.

Katika hatua nyingine, Kamisaa wa CCM Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa huo umepokea zaidi ya Shilingi trilioni 1 na bilioni 400.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Katika miaka 25 iliyopita, mkoa huu ulipokea jumla ya Sh bilioni 285 tu, leo tunazungumza juu ya zaidi ya trilioni moja zilizowekwa kwenye miradi ya maendeleo ndani ya miaka minne,” alisema Babu.

Amebainisha kuwa fedha hizo zimelekezwa kwenye sekta mbalimbali, hasa afya, ambapo ujenzi wa jengo la ghorofa nne la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) umekamilika na limeanza kutoa huduma.

“Wakati tunazungumza juu ya maendeleo, tusiangalie majengo tu bali tuone mabadiliko ya maisha ya wananchi, kwa sasa kina mama wanazalishwa katika mazingira salama, yenye vifaa na huduma bora,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya kitaifa ya Katibu wa NEC wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, inayolenga kusikiliza kero za wananchi, kutoa elimu ya kisiasa na kusisitiza mshikamano ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu ujao.










                                 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.