MOSHI-KILIMANJARO.
WATOA huduma za afya mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuimarisha uelewa na ujuzi wa kutambua viashiria hatarishi kwa wagonjwa mahututi ili kuwezesha utoaji wa huduma za dharura kwa wakati na kuokoa maisha ya wagonjwa.
Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Jairy Khanga, Novemba 18, 2026, mjini Moshi, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa madaktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Medtech Trust, Hospitali ya St. Joseph, Kituo cha Afya Pasua, Hospitali ya Wilaya ya Hai na Hospitali ya TPC.
Dk. Khanga amesema, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa baadhi ya wagonjwa hupoteza maisha kutokana na kukosa huduma za dharura kwa wakati, hali inayoweza kupunguzwa endapo watoa huduma za afya watakuwa na ujuzi wa kutambua mapema viashiria vinavyoashiria kuzorota kwa hali ya mgonjwa.
Amesema mafunzo hayo yanayohusu utambuzi na huduma muhimu za dharura kwa wagonjwa mahututi (Essential Emergency and Critical Care) yanalenga kuwajengea uwezo wataalamu hao kutambua viashiria vya hatari, kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kabla hali zao hazijawa mbaya zaidi.
Dkt. Khanga ameeleza kuwa takwimu za mkoa huo zinaonyesha kuwa kati ya Januari na Oktoba mwaka huu, vifo 17 vilivyoripotiwa vilihusishwa na changamoto za uzazi, ikilinganishwa na vifo 40 vilivyorekodiwa katika kipindi chote cha mwaka 2025.
Hata hivyo, amesema hali imeendelea kuwa ya kutia wasiwasi baada ya vifo vingine 11 kuripotiwa ndani ya mwezi Novemba pekee, na kufanya jumla ya vifo hivyo kufikia 28 tangu Januari mwaka huu.
Amesema ongezeko hilo linapaswa kuwa kichocheo cha kuchukua hatua za haraka kwa kuimarisha uwezo wa watoa huduma za afya katika kutambua viashiria vya hatari na kutoa huduma kwa wakati.
Ameeleza kuwa licha ya Serikali kuendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuwekeza katika vifaa tiba, upatikanaji wa dawa na kuboresha miundombinu ya hospitali, bado kuna umuhimu wa kuimarisha ujuzi wa watumishi ili changamoto za vifo vinavyoweza kuzuilika zipungue.
Ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuyazingatia na kuhakikisha wanatumia ujuzi watakaoupata katika maeneo yao ya kazi ili kuboresha huduma na kuongeza uwezekano wa kuwaokoa wagonjwa.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Dkt. Abdul Issa, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Wizara ya Afya unaolenga kuwawezesha watumishi kupata mafunzo endelevu yatakayoongeza ujuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Amewataka washiriki kuwa mabalozi kwa wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo ili elimu na ujuzi watakaoupata viweze kuwafikia watumishi wengi zaidi.
Naye Mratibu wa mafunzo hayo kutoka TANPA, Prosper Protus, amesema yameandaliwa na Shirika la Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK) kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Usingizi na Ganzi Tiba (TANPA), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Hospitali ya TPC na Taasisi ya Medtech Trust.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi wanaohudumu katika vituo vya afya vya Pasua, St. Joseph, Mawenzi, Hospitali ya Wilaya ya Hai na TPC, ili waweze kutambua mapema viashiria vya umahututi kwa wagonjwa na kuwapatia matibabu stahiki.
Ameongeza kuwa mradi huo umefikia mwaka wa tatu tangu kuanzishwa kwake, huku malengo ya baadaye yakiwa ni kupanua mafunzo hayo kwa watumishi wa sekta ya afya katika mkoa mzima wa Kilimanjaro ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya nchini.
![]() |
![]() |























