WASHIRIKI 600 WAJIANDIKISHA TIDI LUNG HEALTH HALF MARATHON

MOSHI-KILIMANJARO.

ZAIDI ya washiriki 600 wamejiandikisha kushiriki mbio za TIDI Lung Health Half Marathon zinazotarajiwa kufanyika Novemba 8, mwaka huu, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza michezo, kuhamasisha jamii kuhusu afya ya mapafu na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu.

Mratibu wa mbio hizo, Nelson Mrashani, ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, ambapo amesema maandalizi yamefikia asilimia 90 huku idadi ya washiriki ikiendelea kuongezeka kuelekea siku ya mashindano hayo.

Amesema mbio hizo zinalenga kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya, kukuza sekta ya michezo nchini pamoja na kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yanayoathiri mfumo wa upumuaji.

Mrashani amesema pia mbio hizo zitatumika kama fursa ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi maalumu itakayohudumia wagonjwa wa kifua kikuu na wale wanaosumbuliwa na ugonjwa wa silikosisi, unaosababishwa na kuvuta vumbi kwa muda mrefu, hususan katika shughuli za migodini.

Amesema wagonjwa wa magonjwa hayo huhitaji muda mrefu wa matibabu, hivyo uwepo wa wodi maalumu utasaidia kuboresha mazingira ya huduma na kuwawezesha kupata matibabu katika mazingira yanayokidhi mahitaji yao.

Ameongeza kuwa kupitia mbio hizo, waandaaji wanatarajia kukusanya Sh bilioni tatu kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa wodi hiyo, huku akieleza kuwa mashindano hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI), mwaka 1926, na yamekusudiwa kuwa ya kila mwaka.

Aidha, Mrashani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAAA), ameishukuru Serikali kwa kupandisha hadhi iliyokuwa Hospitali Maalumu ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH) na kuifanya kuwa Taasisi kamili, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio hizo ambapo pia atashiriki mbio hizo.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.