KILIMANJARO SPORTS ACADEMY YAPONGEZWA KUFANIKISHA CHANJO KWA WATOTO ZAIDI YA 120

MOSHI-KILIMANJARO.

DIWANI wa Kata ya Korongoni,Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Issah Elias Bulilo, amepongeza uongozi wa shule ya Kilimanjaro Sports Academy kwa kushiriki katika kampeni ya chanjo na kufanikisha watoto120 kupata huduma hiyo, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya juhudi za kulinda afya na ustawi wa watoto.

Aidha, amewapongeza wazazi na walezi wa watoto hao kwa kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo, akieleza kuwa mafanikio hayo yasingeweza kupatikana kwa urahisi bila ushirikiano wao, ikizingatiwa kuwa kuwafikia watoto mmoja mmoja kungekuwa na changamoto.

Bulilo ametoa pongezi hizo leo Ijumaa Oktoba 30, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya tatu ya shule ya Awali na Msingi ya Kilimanjaro Sports Academy, ambapo alisema elimu kuhusu kampeni hiyo ilitolewa katika maeneo mbalimbali kupitia ofisi ya Mtendaji wa Kata na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

"Elimu ya kampeni ya chanjo ilitolewa katika maeneo mengi hapa nchini kupitia ofisi za watendaji wa kata na wakuu wa wilaya, niwapongeze sana uongozi wa shule ya Kilimanjaro Sports Academy kwa kuipokea kampeni hiyo na kufanikisha watoto zaidi ya 120 kupata chanjo," alisema Bulilo.

Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Mwalimu Henry Mallya, kwa maono yake ya kuwekeza katika sekta ya elimu, akisema uwekezaji huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata elimu, sambamba na kupanua wigo wa ajira nchini kupitia taasisi za elimu anazozisimamia.

Adha alisema Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeendelea kufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu, hivyo kuitaka sekta binafsi inayoshirikiana na Serikali katika utoaji wa elimu kuendana na mabadiliko hayo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yanayokidhi mahitaji ya sasa, huku wakijengewa misingi ya maadili mema.

Akisoma risala ya ahule kwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkurugenzi wa shule hizo za Northern Highlands, Henry Mallya, Msimamizi wa shule hizo, Wolter Mallya, aliwashukuru wazazi na walezi kwa imani waliyoendelea kuwa nayo kwa taasisi hiyo kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi darasa la sita.

Alisema ushirikiano wa wazazi katika kufuatilia maendeleo ya taaluma, nidhamu, kutoa ushauri kupitia vikao mbalimbali pamoja na kutekeleza wajibu wa kulipa ada umekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya shule hizo.

Hata hivyo, Mallya aliwataka wazazi ambao hawajakamilisha malipo ya ada kufanya hivyo kwa wakati ili kuwezesha mipango na shughuli za shule kutekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Kilimanjaro Sports Academy Abuu Makande (Teacher Makande), aliwashukuru wazazi kwa kuendelea kuziamini shule nyingine zinazomilikiwa na taasisi hiyo.

Alisema taasisi hiyo inazo shule nyingine zikiwemo The Moshi Academy iliyopo eneo la Stendi ya Mbuyuni, Guardians Angels iliyopo Kata ya Kiusa, Moshi Health iliyopo Sambarai ambayo ni tawi la Moshi Academy lililopo Nyumba ya Magereza, pamoja na shule ya sekondari ya Northern Highlands iliyopo karibu na Uwanja wa Mashujaa.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.