MOSHI-KILIMANJARO.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, kimeanza kuifanyia ukarabati jengo hilo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1977
Ukarabati huo unalenga kuboresha muonekano wa jengo hilo pamoja na miundombinu yake ili kuweka mazingira bora ya utendaji kazi
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maboresho yanayoendelea katika jengo hilo, akieleza kuwa ofisi ya CCM mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kutekeleza mpango huo kuelekea maadhimisho hayo.
Amesema jengo hilo lilijengwa mwaka 1984 na tangu wakati huo halijawahi kufanyiwa marekebisho, hivyo hatua ya sasa inalenga kurejesha na kuboresha miundombinu yake ili iendane na mahitaji ya sasa.
Aidha amesema kamati ya Siasa ya mkoa tayari imetenga bajeti ya Sh milioni 440 kwa ajili ya kullifanyia ukarabati mkubwa jengo hilo kwani miundombinu yake ikiwemo mifumo ya umeme, majitaka imechakaa.
Boisafi amesema kutokana na hali ya jengo hilo kwa sasa linahitaji marekebisho makubwa baada ya kutumika kwa muda mrefu bila kufanyiwa ukarabati mkubwa.
"Jengo la makao makuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro lilijengwa tangu mwaka 1984, tangu wakati huo halikuwahi kufanyiwa marekebisho, kwa sasa linahitaji marekebisho makubwa ikiwemo miundombinu ya umeme, mifumo ya majitaka na ukarabati wa vyumba na maeneo mengine," amesema Boisafi.
Baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM mkoani humo, akiwemo Christopher Kimonge, Ally Mwinyi Ally, Abdallah Mtwenge na Rashidi Mmemo, wameipongeza Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa ukarabati wa jengo hilo, wakieleza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha miaka 50 ya chama hicho na kuboresha mazingira ya ofisi za chama.






