MOSHI-KILIMANJARO.
TIMU za Usimamizi wa Huduma za Afya katika ngazi ya mkoa na wilaya mkoani Kilimanjaro zinataraniwa kushiriki katika warsha ya mafunzo inayolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika huduma za dharura na vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa.
Warsha hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu wa afya kutambua umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za dharura, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika kutoa huduma kwa wagonjwa mahututi.
Mratibu wa Mafunzo wa Chama cha Wataalamu wa Usingizi na Ganzi Tiba (TANPA), Prosper Protus, hayo ameyasema Novemba 19,2026 Mjini Moshi wakati akizungumza na KISENAUPDATED.BLOGSPOT.COM kuhusiana na warsha hiyo.
Amesema uwekezaji katika huduma hizo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.
"Warsha hii ni ya siku moja ambapo itawashirikisha viongozi kutoka halmashauri zote za mkoa wa Kilimanjaro, wakiwemo Waganga Wakuu wa Wilaya, Wauguzi Wakuu, wajumbe wa Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Wilaya (CHMT) na mkoa (RHMT)."amesema.
Aidha amewataja washiriki wengine ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI).
Ameongeza kuwa "warsha hiyo imeandaliwa na Shirika la Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK) kwa kushirikiana na TANPA, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Hospitali ya TPC na Taasisi ya Medtech Trust."





