WANAWAKE WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUPATA ELIMU KABLA YA KUKOPA

MOSHI-KILIMANJARO.

WANAWAKE wajasiriamali wametakiwa kupata elimu ya kutosha kuhusu mikopo kabla ya kukopa, ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kuepuka madeni yasiyo na tija na kukuza biashara zao kwa ufanisi.

Afisa Mahusiano wa Benki ya Azania, Tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro, Aida Mbilinyi, aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya fedha kwa Wanawake wajasiriamali katika Kongamano la Fursa za Biashara na Urasimishaji lililoandaliwa na Chemba ya Biashara ya Wanawake Tanzania (TWCC), mkoani Kilimanjaro.

Amesema wajasiriamali hawapaswi kukopa kwa sababu tu wanahitaji fedha, bali wanapaswa kwanza kufahamu gharama za mkopo, masharti yake na uwezo wao wa kurejesha fedha hizo kabla ya kufanya uamuzi wa kukopa.

Aida amesema wajasiriamali wanapaswa kujua tofauti kati ya mikopo inayotolewa na benki, vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) na vyanzo vingine vya mikopo, ili waweze kuchagua njia inayolingana na mahitaji na uwezo wa biashara zao.

“Usikope kwa sababu tu unahitaji mkopo. Ni lazima kwanza uwe na elimu ya kutosha kuhusu mkopo unaotaka kuchukua, gharama zake na namna utakavyoutumia ili uweze kuleta matokeo chanya katika biashara yako,” amesema Aida.

Aidha, amewataka wanawake kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kuweka akiba na kutenga sehemu ya mapato kwa ajili ya uwekezaji, bila kujali kiwango cha fedha wanachopata. Amesema kuwa na maono ya kifedha ni msingi muhimu wa kufikia malengo ya biashara na kufanya maamuzi yanayozingatia hali halisi ya biashara husika.

Katika mafunzo hayo, Aida amesisitiza mambo matano muhimu yanayoweza kuwasaidia wajasiriamali kusimamia fedha zao, ambayo ni kuandaa bajeti, kuweka akiba, kuwekeza, kufanya maamuzi ya madeni kwa hekima na kuwa na maono ya kifedha.

Mwenyekiti wa TWCC Joyce Ndossi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Kilimanjaro, Joyce Ndossi, amesema kongamano hilo limewakutanisha wanawake wajasiriamali zaidi ya 300 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo kwa lengo la kuwaunganisha, kuwajengea uwezo wa kutambua fursa za biashara na kuwapa uelewa kuhusu sheria na taratibu zinazopaswa kuzingatiwa katika uendeshaji wa biashara.

Amesema kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za kuwasaidia wanawake kuongeza uelewa wa fursa zilizopo, kurasimisha biashara zao na kupata maarifa yatakayowawezesha kuendesha shughuli zao kwa tija na ushindani zaidi.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, Afisa Tawala wa wilaya hiyo, Theresia Mbaga, amewataka wanawake kuamka na kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo badala ya kusubiri fursa hizo ziwafuate

Amesema kuna fursa nyingi katika sekta za biashara, kilimo na usindikaji wa mazao ambazo wanawake wanaweza kuzitumia kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao, huku akiwahimiza kujifunza na kutumia maarifa mapya katika kuendeleza shughuli zao.

Mbaga ameipongeza TWCC kwa kuandaa kongamano hilo, akisema linatoa nafasi kwa wanawake wajasiriamali kupata elimu kuhusu urasimishaji wa biashara na kuboresha bidhaa zao kupitia uelewa wa viwango vinavyosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kongamano hilo la Fursa za Biashara na Urasimishaji limeandaliwa na TWCC kwa lengo la kuwawezesha wanawake katika biashara, likiwa na kauli mbiu isemayo: “Rasimisha Biashara Yako, Fungua Milango ya Fursa.”












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.