JIPENDEA, MWANGA
Wakazi wa vijiji vya Kivisini, Kigonigoni Tarafa ya Jipendea Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, hususan Wanaume wanalazimika kulala mashambani mwao ili kulinda mazao yao yasiharibiwe na wanyamapori haswa tembo.
Wakizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na swala hilo, baadhi ya wananchi hao haswa Wanawake wamesema hakuna njia nyingine iliyoko zaidi ya kulinda mazao hayo ambayo walmeema mengi ya mazao hayo ni yale yaliyobaki mashambani baada ya mengine kuharibiwa na wanyapori hao.
Mkazi wa Jipendea Zulfa Saidi amesema waume zao kwa sasa wanalazimika kulala mashambani kulinda mazao, jambo ambalo linawafanya swao na watoto kukosa haki zao za msingi ambazo zinaambatana na uwepo wa Baba nyumbani haswa nyakati za usiku:
Amesema kuwa mbali na kukosa kuwa karibu na waume zao nyakati za usiku, pia uchumi wa familia unaporomoka kutokana na hali hiyo kwani, Baba ndiyo nguzo ya familia ambapo anawajibika kutoka kwenda kutafuta riziki ya familia, lakini kutokana na hali ya kukesha shambani usiku kucha swala tendo la ndoa hawezi kulifanya mchana maana inabidi apumzike tayari kwa ajili ya kukesha usiku unaofuata.
Wakazi wengine wa eneo hilo Mudhihiri Rajabu na Abutwalib Kajiru, wamesema hata watoto wao, ambao wanawajibika kuamka asubuhi na mapema ili waweze kuwahi mashuleni kwa wale wanaosoma maeneo ya mbali inabidi wachelewe shule maana hawawezi kutoka mapema wakati tembo bado wako maeneo ya makazi.
Naye mkazi wa kijiji cha Kivisini Esther Raphael amesema tembo hao wameweka kambi kwenye kijiji chao ambapo wamegeuza kama uwanja wa kufanyia mazoezi pindi wanaposhiba hawataki kuondoka na wanapomaliza kula mazao, huweka kambi katika eneo hilo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kivisini Mwalimu Ziada Mziray, ameiomba Serikali kujenga kituo cha kuwafukuza wanyama hao ili wananchi wapate unafuu wa kuyalinda mazao yao, pamoja na kuwapatia vifaa vya vipulizi ili wananchi wanapowaona tembo hao waweze kuwafukuza.
Akijibu swali la waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea na jitihada za kuwadhibiti tembo hao kwa kuwarudisha kwenye hifadhi pindi wanapotoka kuvamia maeneo ya wananchi.